Jumamosi 6 Septemba 2025 - 23:40
Rais wa Baraza la Maimamu wa Kishia Pakistan: Mafundisho ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w) ndiyo funguo ya umoja na suluhisho la Umma wa Kiislamu

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, katika hotuba zake, amesisitiza kwamba njia pekee ya kueoukana na machafuko na kuifikia jamii yenye umoja na yenye mafanikio ni kushikamana na mafundisho na mwenendo wa Mtume Mtukufu Muhammad Mustafa (s.a.w.w).

Kwa mujibu wa kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, sambamba na kuwadia Wiki ya Umoja, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Maimamu wa Kishia Pakistan, alituma pongezi kwa Waislamu wote kutokana na mnasaba wa siku hizi tukufu na akasisitiza: Njia pekee ya kurekebisha hali mbaya na ufisadi katika nyanja mbalimbali za maisha ni kurejea katika mafundisho na mwenendo wa Mtume wa heshima wa Uislamu, Bwana Muhammad Mustafa (s.a.w.w).

Katika maneno yake alieleza: Uwepo mtukufu wa Mtume (s.a.w.w) ni mkusanyiko wa sifa bora na ukamilifu wa kibinadamu, na mwenendo wake wenye nuru si kwa ajili ya Umma wa Kiislamu pekee, bali ni kielelezo kamili na cha milele kwa wanadamu wote.

Msomi huyu mashuhuri wa Pakistani, akirejelea umuhimu wa kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu, alibainisha: Sherehe ya kuzaliwa kwa Khatamul-Anbiya (s.a.w.w) inapaswa kufanyika kwa taadhima na utukufu, lakini sambamba na furaha na shangwe, tusisahau ujumbe mkuu wa tukio hili; bali tunapaswa kuyafanya mafundisho na maagizo ya Mtume kuwa taa ya mwongozo katika nyanja zote za maisha, na tuondoe upotovu na kutoshikamana na mwenendo wake.

Akaongeza kuwa: Maisha ya Mtume wa Uislamu na tabia zake tukufu zinatutaka sisi, kwa mwanga wa mafundisho ya Kinabii, kuimarisha mshikamano miongoni mwa Waislamu, kuziboresha kasoro zilizopo katika mifumo na taasisi, na kwa kusonga katika njia ya uadilifu na mshikamano, kuijenga jamii yenye ustawi na yenye mafanikio.

Rais wa Baraza la Maimamu wa Kishia Pakistan aliendelea kusisitiza: Wakati tunaamini kwa yakini kwamba Waislamu wote wana Mungu mmoja, Mtume mmoja, Qur’ani moja na Qibla kimoja, haifai kugawanyika kwa sababu ya mambo madogo na tofauti ndogo; bali tofauti hizo zinapaswa kujadiliwa katika uwanja wa kielimu kwa utulivu, ustahimilivu na kwa adabu na heshima ya hali ya juu.

Alikumbusha pia: Maraaji‘ wakuu wa Taqlid na maulamaa wakubwa daima wamesisitiza kwamba kudhalilisha matukufu ya madhehebu yoyote ya Kiislamu hakujuzu na ni lazima kuepukwa.

Hujjatul-Islam Sayyid Sajid Naqvi mwishoni alibainisha: Leo hii Umma wa Kiislamu unapaswa kwa vitendo kuonesha umoja na mshikamano, na kuthibitisha kwamba wao ni Ummah mmoja, na katika kivuli cha mafundisho ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w) wanaweza kuwa kielelezo cha amani, uadilifu na undugu kwa duniani kote.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha